Okwi;Yanga mkija taifa Octoba 12 mmeumia
EMMANUEL Okwi amejiaminisha kwamba ana uhakika
wa kuishinda Yanga kisheria na kuvaa jezi ya Simba kuanzia Septemba 20
siku utakapoanza msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Hiyo ni tisa tu, kumi ni kwamba ametoa kauli moja
mbaya kwa Yanga akisema: “Oktoba 12 Yanga msije Uwanja wa Taifa,
nitawamaliza.”
Simba na Yanga zitakutana siku hiyo katika uwanja
huo jijini Dar es Salaam katika mechi ya kwanza ya msimu mpya na Mganda
huyo amesema yatawakuta kama ya mwaka 2012.
Mwaka huo katika mechi ya ligi Simba ilishinda
mabao 5-0 ambapo Okwi alifunga mabao mawili, mengine yalifungwa na kipa
Juma Kaseja, Felix Sunzu na Patrick Mafisango (marehemu). Lakini Okwi
ndiye aliyesababisha yote.
Okwi amesajiliwa Simba kwa mkataba wa miezi sita
huku Yanga ikiwashtaki Simba na Okwi Shirikisho la Soka la Tanzania
(TFF) kwa madai ya kukiuka taratibu za usajili ikisema Okwi bado ni
mchezaji wake na inataka kulipwa fidia ya Dola 500,000 (Sh 825 milioni).
Akizungumza na Mwanaspoti kwenye kambi ya Mnyama
mjini hapa, Okwi alisema: “Yanga wasubiri mabao mengine na inaweza kuwa
zaidi ya yale matano, najua wanachotaka kunifanyia Yanga na walianza
muda mrefu, lakini nataka kuwaambia kwamba nitacheza Simba na
sitafungiwa popote.
“Nasubiri siku ya kwenda kusikiliza hiyo kesi na
wasipoangalia watanilipa wao fedha ambazo wanataka mimi niwalipe, kwani
wao ndio waliovunja mkataba wangu.
“Kwanza nilikumbana na adhabu ya kufungiwa, mimi
ningechezaje na sababu hiyo pia walitumia kama kigezo cha kutonilipa
mishahara yangu na mkataba wangu unasema wasiponilipa mishahara yangu ya
miezi mitatu wanakuwa wamevunja mkataba, ngoja tusubiri tuone.
“Kauli za Yanga zinanifanya niwe na hamu kubwa ya
kucheza juu ya kiwango na kufunga mabao mengi, msimu ujao wasipoangalia
watarudia kumbukumbu ya kufungwa goli nyingi sana.”
Kocha wa Simba, Patrick Phiri alisema: “Hili suala
lipo chini ya viongozi wa klabu na tayari limefika TFF ambacho ni
chombo kikubwa cha soka hapa nchini, lakini naweza kusema tu kwa upande
wangu kwamba si vyema mchezaji akakaa nje muda mrefu bila kucheza kwani
kiwango chake kitafifia.
“Wachezaji wengi wana umri mdogo, haipendezi
kabisa kuona kijana mwenye miaka 25 hawezi tena kucheza. Siku hizi
wachezaji hawadumu mchezoni zaidi ya miaka mitano, naamini suala la Okwi
litashughulikiwa na kumalizika ili acheze.
“Okwi ni mchezaji mzuri sana labda tu ujana
unamsumbua, nimezungumza naye naamini amenielewa kwani ana uwezo mkubwa
wa kucheza soka, nataka ndani ya timu wachezaji wote wawe na nidhamu
sawa.
“Mchezaji asipokuwa na nidhamu kwangu hawezi kupata nafasi ya kucheza.”
“Mchezaji asipokuwa na nidhamu kwangu hawezi kupata nafasi ya kucheza.”
Okwi;Yanga mkija taifa Octoba 12 mmeumia
Reviewed by CapchaMuzic
on
03:38:00
Rating: