Bi Harusi Apandisha Mashetani Kanisani!
Chande Abdallah na Deogratius Mongela
Mshtuko! Bi harusi Agnes
Omari (26) amezua kizaazaa baada ya kudaiwa kupandisha mashetani
kanisani wakati akivishwa pete ya ndoa, hali iliyosababisha tendo la
kufungishwa ndoa kusimama kwa muda kwa ajili ya kutafuta msaada wa
maombi.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, bwana harusi,
Arnold Martin alisema sakata hilo lilijiri hivi karibuni kwenye Kanisa
Katoliki la Parokia ya Mbagala-Zakhem jijini Dar.
Alisema
kwamba, alipata taarifa usiku wa kuamkia siku ya ndoa kutoka kwa
msimamizi wa bi harusi kuwa mchumba’ke amepandisha mashetani, tatizo
ambalo hakuwa nalo katika kipindi chote walichoishi pamoja.
Kutokana
na tatizo hilo, Arnold alisema alivunja utaratibu na kwenda kumuona
mchumba’ke huyo na kumkuta akijigaragaza huku akipiga makelele na
kuzungumza lugha za ajabu.
“Kulipokucha, hali yake
ilionekana kuwa nzuri kiasi kwamba majira ya saa 3:00 asubuhi, aliondoka
na msimamizi wake kwa ajili ya kubadilisha gauni la harusi maeneo ya
Mbagala-Kizuiani baada ya lile la awali kuonekana kumbana huku na mimi
nikijiandaa kwenda saluni,” alisema Arnold.
Baada ya kutoka na
msimamizi wake huyo, haukupita muda mrefu akapigiwa simu kuwa hali hiyo
imejirudia, akamfuata na kumbeba kwenye gari lake kisha kumkimbiza
katika Parokia ya Mbagala-Zakhem kwa ajili ya msaada wa maombi na kutoa
taarifa kwa paroko kuhusu hali ya mchumba’ke huyo.
Bi
harusi huyo aliombewa lakini wakati akimvisha pete ya ndoa kanisani hapo
hali hiyo ilijirudia ndipo alipohamishiwa katika Kanisa la Nabii Yaspi
lililopo Buza-Kipera jijini Dar ambapo wakiwa huko, walikutana na
wachungaji ambao waliwaombea na hali ikatulia.
“Hali
hiyo ilijirudia tena wakati tukipiga picha palepale kanisani akaanza
tena kupandisha mashetani, akaombewa lakini hali ilizidi kuwa mbaya,
wakaja watu wa Karismatiki nao ikashindikana ikabidi tufunge safari tena
kuelekea kulekule kwa Nabii Yaspi ambako aliombewa, akapona.
“Wakati
tukiingia ukumbini, hali hiyo ilijirudia tena ambapo sherehe nzima
iliharibika na kuwa majonzi hivyo kila mtu akaondoka kimyakimya.
“Bi
harusi aliondoka na ndugu zake usiku ule hadi kesho yake nilipoambiwa
amerudia hali yake ya kawaida ila kinachonishangaza nilipoenda pale
nyumbani kwao alikuwa akionesha kama vile hanifahamu kabisa pamoja na
kwamba nilifunga naye ndoa,” alisema Arnold ambaye alidai kuwa
anatarajia kurudi tena kwa Nabii Yaspi ili kumaliza tatizo hilo.
Bi Harusi Apandisha Mashetani Kanisani!
Reviewed by CapchaMuzic
on
00:22:00
Rating: