Ukichukua fedha benki sasa ni roho mkononi
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Ni roho mkononi. Hayo ndiyo
maneno matatu yanayofaa kuelezea hali ilivyo jijini Dar es Salaam na
maeneo kadhaa nchini kwa sasa, hasa pale mtu anapobeba fedha nyingi.
Matukio ya ujambazi kwa kutumia silaha yamekuwa
sugu na kusababisha wananchi wanaopeleka au kutoa fedha benki kuvamiwa,
kujeruhiwa au kuuawa mchana kweupe na majambazi wanaotumia pikipiki.
Wananchi wamekuwa wakihoji ni kwa jinsi gani majambazi hao hupata taarifa za mtu aliyekwenda benki ama kuweka au kuchukua fedha.
Mkazi wa Tabata Kimanga, Dar es Salaam, Salum
Mashati alisema: “Haiingii akilini, utasikia mtu kaporwa fedha akitoka
benki. Eti majambazi wanasema kabisa toa hizo milioni 20, wanajuaje kuwa
una kiwango hicho? Huenda watu wa benki wanashiriki uhalifu huu.”
Hata hivyo, meneja wa tawi moja la benki lililopo
Mlimani City, ambaye hakupenda jina lake litajwe alikanusha madai
hayo... “Si kweli kwamba benki zinashirikiana na majambazi kufanya
uhalifu huu. Kwanza wahudumu (bank tellers) hawaruhusiwi kuingia na simu
wanapohudumia wateja.
“Hata mteja anapoingia benki hukatazwa kuongea na
simu au kuandika ujumbe. Mazingira tuliyojiwekea hayaruhusu kabisa
mawasiliano kati ya benki yetu na watu wa nje wakati wa kazi. Nadhani
vitendo hivi vya ujambazi vinaanzia kwa wateja wenyewe kutoa taarifa juu
ya mipango yao kwa watu ambao si waaminifu,” alisema.
Kauli ya Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius
Wambura alitupa lawama kwa wananchi akisema wamekuwa hawaombi ulinzi wa
polisi wakati wa kupeleka au kuchukua fedha benki.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova aliwahi kutoa wito pia kwa taasisi za fedha kulindwa na
polisi badala ya walinzi binafsi.
“Wakuu wa benki wanaogopa gharama za ulinzi kwa
jeshi la polisi ili kuhakikishiwa usalama lakini mwishowe wanaibiwa
kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya kile ambacho wangelipa kwa polisi,”
alisema.
Baadhi ya matukio
Juni 23, mwaka huu, Sista wa Shirika la Mtakatifu
Maria, Parokia ya Mwenyeheri Anwarite, Makoka, Dar es Salaam, Clecensia
Kapuli aliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi wakati akitoka Benki ya
CRDB, Tawi la Mlimani City na kuporwa fedha.
Agosti 8, mwaka huu, Meneja wa Kampuni ya ununuzi wa korosho na
ufuta ya Olam, Jaffari Mgumba aliporwa Sh47 milioni baada ya kuchukua
fedha za ushirika katika Benki ya DTB Tawi la Quality Plaza.
Mtu mwingine ambaye jina lake halikufahamika
alichukua mkopo wa Sh10 milioni, lakini kwa bahati nzuri, kiasi fulani
cha fedha kilibaki benki na kingine akafanya malipo palepale na wakati
anaondoa akiwa amebaki na Sh2 milioni alivamiwa na majambazi waliomtaka
awapatie Sh10 milioni alizochukua.
Tukio jingine la hivi karibuni ni kuuawa kwa
mmiliki wa Kampuni ya Sowers African iliyopo mkabala na Mlimani City,
Adson Cheyo Agosti 22, mwaka huu alipokuwa akitoka Benki ya KCB kuchukua
na kuporwa fedha hizo.
Kabla ya tukio hilo, kulikuwa na ujumbe uliokuwa
ukisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukionya watu kutembea na fedha
nyingi katika maeneo ya Mlimani City, Millennium Tower na Kibo Complex
kwa madai si salama.
Ukichukua fedha benki sasa ni roho mkononi
Reviewed by CapchaMuzic
on
04:14:00
Rating: