Mambo saba makubwa yaliyojionyesha Simba, Yanga huko visiwani Zanzibar




YANGA ilirejea jana Alhamisi kutoka Zanzibar ilikoweka kambi ya siku 10 wakati Simba wameendelea na kambi yao visiwani humo hadi kitakapoeleweka. Yanga inarejea ikiwa imecheza mechi tatu za kirafiki. Ilicheza dhidi ya Chipukizi na kushinda 1-0, dhidi ya Shangani na kushinda 2-0 kabla ya kuizamisha KMKM hapo juzi kwa mabao 2-0.
Simba nayo imecheza mechi mbili za kifariki mpaka sasa na imepanga kucheza nyingine nyingi zaidi visiwani humo. Ilicheza dhidi ya Kilimani na kushinda 2-1 kabla ya kuizamisha Mafunzo kwa mabao 2-0.
Mechi hizo za kirafiki visiwani humo zinatoa ujumbe fulani kwa wadau wa soka nchini. Yafuatayo ni mambo saba ambayo yameonekana katika mechi hizo.
Yanga haijapoteza hela  kwa Coutinho
Moja ya vitu vilivyokuwa vikisubiriwa na wadau wa soka ni kuona cheche za Wabrazili wa Yanga. Wabrazili hao Andrey Coutinho na Genilson Santos ‘Jaja’ wamesajiliwa msimu huu na kuwa wachezaji wa kwanza kutoka Amerika Kusini kucheza Yanga. Katika mechi tatu za kirafiki Yanga ilizocheza visiwani Zanzibar Mbrazili Coutinho amedhihirisha kuwa hajaja nchini kubahatisha. Amefunga mabao mawili, pia amecheza kwa kiwango cha juu na kuibua hamasa kubwa kwa wapenzi wa Yanga na soka kwa ujumla. Kwa kiwango alichoonyesha Coutinho mpaka sasa ni dhahiri kuwa dola 15,000 (Sh 24.3 milioni) zilizotumiwa na Yanga kumsajili mshambuliaji huyo hazijaenda na maji.
Tegete, Bahanuzi watarejea benchi
Wapenzi wengi wa soka nchini waliamini kuwa ujio wa Mbrazili Marcio Maximo kwenye kikosi cha Yanga huenda ukarejesha makali ya straika Jerry Tegete lakini hali inaonekana kuwa tofauti. Tegete alicheza kwenye kikosi cha Taifa Stars na Maximo kwa mafanikio lakini sasa maisha yanaonekana kubadilika. Hali pia si nzuri kwa straika mwingine Saidi Bahanuzi ambaye wadau wa soka nchini hawaamini kama amefulia, wengi wanatarajia kuwa atarejea kwenye makali yake.
 Tegete na Bahanuzi wote wamecheza mechi zote tatu za kirafiki Yanga ilizocheza visiwani Zanzibar lakini hakuna hata mmoja kati yao aliyeweza kuzifumania nyavu. Straika mpya wa kikosi hicho Mbrazili Jaja amewafunika kwa kufunga bao moja licha ya ugeni wake kwenye kikosi hicho huku Hussein Javu ambaye anapewa nafasi ndogo ya kufanya vizuri naye akiwa amezifumania nyavu. Ni dhahiri kuwa kwa mwendo huu Tegete na Bahanuzi watabisha hodi tena benchi walipopazoea.
Phiri amepandisha morali Simba
Wachezaji wa Simba walikuwa wanacheza tu bila malengo wakati kocha Zdravko Logarusic alipokuwa na kikosi hicho. Viongozi wa Simba waliamua kuachana na Logarusic na kumleta Mzambia Patrick Phiri anayekinoa kikosi hicho kwa sasa. Simba tayari imeshinda mechi zote mbili za kirafiki ilizocheza dhidi ya Kilimani City na Mafunzo. Wachezaji wa kikosi hicho wanaonekana kucheza kwa kujituma na kujitoa. Hiyo ilikuwa tofauti wakati akiwa Logarusic. Kwa hali hiyo inaonekana kuwa ujio wa Phiri umepandisha morali ya wachezaji wa kikosi hicho na huenda msimu ujao wakawashangaza wengi.
Tambwe si tegemeo tena Simba
Straika Mrundi Amissi Tambwe alikuwa tegemeo kwenye kikosi cha Simba msimu uliopita, alifunga mabao 19. Mechi bila Tambwe ilikuwa ngumu kwa Simba kwani umaliziaji wa kikosi hicho ulikuwa butu. Mpaka sasa Simba imecheza mechi mbili na kushinda zote, waliifunga Kilimani City mabao 2-1 kabla ya kuifunga tena Mafunzo mabao 2-0. Tambwe hajafunga bao lolote kati ya hayo. Ni dhahiri kuwa kikosi cha Simba kimeanza kuwa na mabadiliko, wafungaji wameongezeka. Straika mpya wa kikosi hicho Elius Maguli amefunga bao moja, kiungo mpya Shabani Kisiga naye kafunga, Haruna Chanongo kafunga mawili. Ni uwezo mkubwa. Tambwe anatakiwa kuelewa kuwa maisha yamebadilika na anatakiwa kujituma zaidi kwaajili ya msimu ujao.

Chanongo ameanza kuimarika
Malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na aliyekuwa kocha wa Simba, Zdravko Logarusic ni kuwa mshambuliaji Haruna Chanongo amekuwa na homa za vipindi. Amekuwa akifanya vizuri mechi moja na kupotea inayofuata. Chanongo amefunga bao moja kwenye kila mechi aliyocheza, ameonyesha kiwango. Ni dhahiri kuwa mshambuliaji huyo ameanza kuimarika na anaweza kufanya makubwa msimu ujao.
Twite, Omega wameziba pengo la Domayo
Viraka Mbuyu Twite na Omega Seme wameonekana kuimarika katika nafasi ya kiungo na huenda wakawasahaulisha Wanayanga machungu ya kuondokewa na kiungo wao mahiri Frank Domayo. Kuondoka kwa Domayo kulionekana kuleta hofu lakini kiwango kilichoonyeshwa na Twite pamoja na Omega katika nafasi hiyo ni dhahiri kuwa pengo lake linaonekana kuzibwa.
Mbeya City ina malengo makubwa
Simba na Yanga zimecheza visiwani Zanzibar ambako ni mbali kidogo kutoka Tanzania bara. Ni mbali zaidi kutoka mikoa ya kusini kama Mbeya hadi Zanzibar. Umbali huo si kitu kwa Mbeya City kwani ilimtuma kocha wa kikosi hicho Juma Mwambusi kwenda kuzifanyia ushushushu Simba na Yanga. Ni kocha pekee wa timu za Ligi Kuu aliyekwenda visiwani humo. Ziara hii ya Mwambusi inatoa ujumbe kuwa kikosi chake cha Mbeya City kimepania kufanya makubwa msimu ujao. Kimepania kuzipiku Simba na Yanga. Ni ujumbe kuwa timu hiyo ina malengo makubwa tofauti na inavyodhaniwa.
Mambo saba makubwa yaliyojionyesha Simba, Yanga huko visiwani Zanzibar Mambo saba makubwa yaliyojionyesha Simba, Yanga huko visiwani Zanzibar Reviewed by CapchaMuzic on 00:49:00 Rating: 5
Powered by Blogger.