Uenyekiti wa Rais Magufuli CCM Waiva, Kamati Kuu ya Chama Hicho Kukutana Dar es Salaam Kesho

Maandalizi ya CCM kumkabidhi Rais John Magufuli uenyekiti wa chama hicho ili ashike kofia zote mbili, yataanza kesho katika kikao cha Kamati Kuu kilichopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam.

Taarifa kuhusu kikao hicho iliyotiwa saini na msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka ilisema: “Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM itafanya  kikao cha kawaida siku ya Jumamosi jijini Dar es Salaam. Kikao hicho kitafanyika chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais mstaafu Jakaya Kikwete.”

Japokuwa taarifa hiyo haikueleza ajenda za kikao, habari kutoka ndani ya chama zinasema kikao hicho cha siku moja kinatarajiwa kujadili masuala mbalimbali, ukiwamo mchakato wa makabidhiano ya kiti hicho katika mkutano mkuu wa chama hicho utakaofanyika mwezi ujao.

Kipindi cha uongozi wa chama kwa Kikwete kitamalizika mwakani, lakini imekuwapo desturi kwa rais mpya kuachiwa kofia hiyo mapema, hivyo Rais Magufuli anatarajiwa kurithi mikoba ya uenyekiti mwezi ujao.

Vilevile, kikao hicho kinatarajiwa kuhitimisha hoja zinazodaiwa kuibuka katika vikao vya ndani vya chama hicho kwamba CCM inataka kuvuruga utaratibu uliodumu kwa muda mrefu wa mwenyekiti kumwachia kijiti Rais aliyeko madarakani.

Madai kuhusu mkakati huo wa ndani yalisambazwa katika mitandao ya kijamii yakimnukuu Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, lakini Ole Sendeka alisema hana sababu yoyote ya kumjibu kiongozi wa dini.

Februari 5, mwaka huu Kikwete alipokuwa anazungumza na wazee wa Manispaa ya Singida alisema sherehe za mwaka huu za maadhimisho ya miaka 39 tangu chama hicho kuanzishwa zilikuwa za mwisho kwake akiwa mwenyekiti, kauli ambayo iliashiria ataachia mapema uenyekiti.

Kwa desturi, wenyeviti wa CCM huwa wanaachia madaraka yao kabla ya muda wa uongozi wao kumalizika.

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alikabidhiwa chama na Alhaji Ali Hassan Mwinyi mwaka 1996 badala ya 1997 na Mkapa alimkabidhi Kikwete kiti hicho mwaka 2006 badala ya 2007.

Kulingana na kalenda ya chama hicho, Mkutano Mkuu wa CCM kumchagua mwenyekiti unapaswa kufanyika mwaka 2017, lakini utafanyika mwaka huu kuendeleza utamaduni wa kung’atuka mapema.

Habari kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa kinachoendelea sasa mikoani na wilayani ni maandalizi ya mkutano huo mkuu yanayosimamiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Bara, Rajabu Luhwavi kwa niaba ya Sekretarieti.

“Kikao hicho cha Kamati Kuu ndicho kitakachojadili ajenda za mkutano huo sambamba na kupanga tarehe ya kufanyika kwa mkutano mkuu,” zilieleza taarifa hizo.

Dk Magufuli anatajwa kuwa uongozi wake ndani ya CCM utakuwa wa kasi ya aina yake kutokana na hatua mbalimbali za ‘utumbuaji majipu’ anazozifanya ndani ya Serikali tangu Novemba 5, alipoapishwa kuwa Rais.
Uenyekiti wa Rais Magufuli CCM Waiva, Kamati Kuu ya Chama Hicho Kukutana Dar es Salaam Kesho Uenyekiti wa Rais Magufuli CCM Waiva, Kamati Kuu ya Chama Hicho Kukutana Dar es Salaam Kesho Reviewed by Unknown on 00:04:00 Rating: 5
Powered by Blogger.