Polisi wanamhujumu Rais Magufuli

Kitendo cha Polisi kuwazuia wana CHADEMA kumuaga na hatimaye kumpuzisha kiongozi wao Alphonce Mawazo, ni cha kulaaniwa. Hii ni hujuma ya Polisi inayochochea hasira za wananchi kwa Serikali hii mpya ambayo walau imeanza kuonyesha matumaini ya kuaminiwa.
Mawazo kauawa kama walivyouawa wana mapinduzi wengi katika Tanzania, Afrika na Dunia. Hatukusikia polisi wakizuia Samora Machel aagwe eti kwa hofu kwamba wananchi wangefanya vurugu kutokana na chuki zao kwa makaburu waliodungua ndege yake.
Hatukusikia Martin Luther King, watu wakizuiwa kumuaga kwa hofu eti Wamarekani weusi na wapinga ubaguzi wangefanya vurugu.
Hatukuona Watanzania wakizuiwa kumuaga Edward Sokoine aliyekufa katika ajali iliyosababishwa na mkimbizi wa Afrika Kusini, kwa hofu ya wananchi kulipiza kisasi.
Mawazo ameuawa. Kuna madai, nasisitiza madai, kwamba CCM wamehusika katika kifo hicho. Hatujaona polisi wakihangaika kuwasaka wauaji kama wafanyavyo katika matukio mengine mengi. Hatujasikia salaam za rambirambi na za kulaani mauaji hayo kutoka CCM au Serikalini.
Makabwela wafuasi na wapenzi wa Mawazo hawana namna ya faraja. Wameamua kumuaga kiongozi wao kwa heshima na kuonyesha mshikamano. Wanazuiwa.
Dk. Magufuli aliahidi kuwa Watanzania wote ni wake bika kujali itikadi zao. Nadhani katika hili ni busara tu inayohitajika. Polisi waimarishe ulinzi ili CHADEMA wapate haki yao ya asili kabisa ya kutoa heshima za mwisho kwa mpendwa wao.
Kuwazuia CHADEMA kutakuwa ni kazi ya polisi ya kuifanya Serikali hii ichukiwe, hasa ikizingatiwa Geita ndiko anakotoka Rais wetu. Polisi watumie busara.
Wasitumike kama roboti.
Nawasilisha kama mzalendo.
Polisi wanamhujumu Rais Magufuli
Reviewed by CapchaMuzic
on
00:18:00
Rating:
