DIAMOND Kuna Ulazima Gani Kuishi na Mama Yako Katika Umri Huo? Sio Kosa ila Kuna Ulazima wa Kujitenga..

KWAKO mkali wao katika anga la Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’. Mambo vipi mzazi jembe? Hongera sana kwa ushindi mnono ulioupata hivi karibuni katika Tuzo za MTV EMA 2015 jijini Milan Italy, umezidi kuliletea taifa letu heshima.

Ukitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima. Namshukuru Mungu naendelea kupambana na kazi zangu kama kawaida ili mkono uende kinywani.Nimekukumbuka leo kwa barua kwani kuna jambo nataka nikushauri. Ikiwezekana ulichukulie hatua fasta na nina amini heshima yako itazidi kuongezeka hususan katika eneo la uhusiano na baadaye ndoa.

Natambua jinsi gani unampenda mama yako. Najua mama kwako ndiyo kila kitu na ndiyo maana unatamani kukaa naye karibu. Unatamani wakati mwingine hata usiende kufanya shoo ili uwe karibu naye, lakini unashindwa tu pale unapobanwa na majukumu ya kimuziki.

Muziki unakutenganisha na mama kwa sababu ni kazi lakini vinginevyo, ungekuwa mtu wa kushinda naye nyumbani. Pamoja na mapenzi hayo kwa mama yako mzazi, hadhi uliyonayo sasa hivi kama msanii mkubwa au namba moja Bongo, sioni kama kuna sababu ya kuendelea kukaa nyumba moja na mama, japo una nia njema kufanya hivyo.

Familia zetu za kiswahili tunajuana, sisemi kwamba ukikaa na mama huku ukiwa na mpenzi wako au mkeo ni makosa, lakini mimi naona ni busara zaidi ukawa mbali na mama yako. Ikiwezekana kama hiyo nyumba mnayoishi umemjengea yeye, basi ni bora wewe ukakae sehemu nyingine ili uwe huru zaidi.

Tumeshuhudia hivi karibuni kuondoka kwa mpenzi wako, Zarinah Hassan ambaye amerudi kwake nchini Afrika Kusini. Nyuma yake kulikuwa na maneno ya hapa na pale. Ikasemekana kuna mambo yalikuwa hayaendi sawa, ‘figisufigisu’ za mawifi sambamba na mama’ko zilikuwa zikitokea.

Hayo manenomaneno yasingeweza kutokea kama ungekuwa unakaa mbali naye. Umemjengea mama nyumba nzuri lakini si lazima mkae pamoja. Wewe waweza hata kupanga, mama yako akabaki hapo akainjoi maisha.
Wewe unahitaji kuwa na mji wako. Uwe na familia yako ambayo inajitegemea, hivyo ni busara zaidi ukajitenga na mama, si kwa nia mbaya lakini yeye inapendeza zaidi kama utakuwa unakwenda kumsalimia tu kadiri uwezavyo na hata yeye kuja kwako kukusalimia pale anapojisikia.

Faragha yako na mkeo ni nzuri ikaheshimika. Mjiachie wenyewe na watoto wenu mtakaojaliwa. Inapendeza watoto nao wakifunga safari kwenda kumsalimia bibi yao. Hayo ndiyo maisha mazuri, tena yenye hadhi yako kama staa namba moja Bongo.

Ni matumaini yangu utakuwa umenielewa mzazi na nikusihi ulifanyie kazi suala hilo maana linaleta heshima kwako na linasaidia kuondoa migogoro ya hapa na pale ambayo naamini kabisa inaepukika.
Nikutakie maisha marefu yenye baraka na uendelee kutupa burudani kwani umezaliwa kutuburudisha!
Ni mimi nduguyo,

By Erick Evarist/GPL
DIAMOND Kuna Ulazima Gani Kuishi na Mama Yako Katika Umri Huo? Sio Kosa ila Kuna Ulazima wa Kujitenga.. DIAMOND Kuna Ulazima Gani Kuishi na Mama Yako Katika Umri Huo? Sio Kosa ila Kuna Ulazima wa Kujitenga.. Reviewed by CapchaMuzic on 02:31:00 Rating: 5
Powered by Blogger.