Mama Kanumba Atoa ya Moyoni ''Lulu alipenda Kanumba Aondoke Ili Yeye Apate Mafanikio''
Staa wa Bongo Movies, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mama wa aliyekuwa nyota wa fani hiyo, Steven Kanumba, Flora Mtegoa wamefikia pabaya baada ya mama huyo kumshushia Lulu maneno makali na ya shutuma.
Kwa mujibu wa Gazeti la Amani, inadaiwa kuwa mama Kanumba amemlalamikia Lulu kwamba, amemtupa na kumtenga tofauti na zamani ambapo uhusiano wao ulikuwa kama wa mama na binti yake.
Akizungumzia swala hilo kwa njia ya simu mama Kanumba alilieleza gazeti hilo kinaga ubaga
“Lulu si Lulu yule jamani. Lulu sasa hivi amebadilika. Awali aliniambia hatanitupa, lakini sivyo. Lulu siku hizi haji kunisalimia wala hanipigii simu.”
“Imefika mahali nawaza kwamba, huenda alipenda Kanumba aondoke ili yeye apate mafanikio makubwa aliyonayo sasa. Lulu amenitenga, amenitenga, amenitenga!” , Mama Kanumba alisema.
Juzi, Jumanne, ambayo ilikuwa siku ya kuadhimisha mwaka wa tatu tangu kifo cha staa huyo, mama huyo alishiriki kwa kwenda kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar kwa lengo la kusafisha kaburi la mtoto wake. Baada ya zoezi la kusafisha kaburi kumalizika, mama Kanumba aliongea na Amani na kuyasema haya:
“Nasikitika sana namna ambavyo Lulu amekuwa tofauti na maneno yake ya zamani kwamba atakuwa sambamba na mimi katika kuadhimisha kumbukumbu ya Kanumba. Lakini leo kama hivi, hajatokea.
“Pia nasikitishwa na kitendo cha kufanya bethidei ya mdogo wake jana (Jumatatu usiku) kule Posta wakati anajua ndiyo usiku ambao Kanumba alifariki dunia.
“Mbaya zaidi, akiulizwa na watu kwa nini sasa hivi hayupo sambamba na mimi kama zamani, anajibu majibu ambayo hayaeleweki. Kumbe maneno yake ya zamani kwamba atakuwa sambamba na mimi yalikuwa ya usaliti.
“Kwa hiyo na mimi sasa nimeamua kubaki peke yangu kama nilivyo, nitaendelea kumuenzi Kanumba mwanangu kwa sababu mimi ndiyo mama yake kwa hiyo nalia peke yangu.”
Katika mazungumzo yake, mama Kanumba alikwenda mbali zaidi kwa kusema: “Kuna siku aliahidi kwamba atajengea picha ya Kanumba ikiwa ndani ya kioo na kuiweka juu ya kaburi, hajafanya hivyo. Nitafanya mwenyewe.“Labda amepuuza kwa vile anajiona anazidi kukua kisanii, ni supastaa ndiyo maana anatoa ahadi za uongo.”
Lulu alipotafutwa juzi na gazeti hilo kuzungumzia malalamiko ya mama mkwe wake huyo, hakupatikana lakini wiki iliyopita alizungumza na paparazi wetu kuhusu mtazamo wa maisha yake kwa jumla ambapo alisema:“Mimi kwa sasa hivi nina mtazamo mwingine kabisa kuhusu maisha. Kwanza sidhani kama nitamwaga machozi tena kuhusu Kanumba maana nimelia sanasana.“Mtu ambaye naweza kumlilia ni mama yangu (Lucresia Karugila) na mdogo wangu. Lakini si mtu mwingine. Kwa sasa naangalia zaidi familia yangu.”
Mama Kanumba Atoa ya Moyoni ''Lulu alipenda Kanumba Aondoke Ili Yeye Apate Mafanikio''
Reviewed by CapchaMuzic
on
01:28:00
Rating: