“Sijui walitumia gundi ya aina gani kumbandikia kucha mwanangu, mpaka sasa sielewi, mtoto mwenyewe ndiyo huyo huyo mmoja wa kike niliyekuwa nikimtegemea na ndiyo kwanza ndoa yake bado change kabisa hata mwezi mmoja haina, huu ni mtihani mkubwa kwangu na kwa mumewe ambaye wamefunga naye ndoa wiki tatuzilizopita, inauma sana lakini tunamwachia Mungu.”

Picha ya Marehemu

Ni maneno ya mama mzazi wa Sophia Komba aliyefariki dunia hivi karibuni jijini Dar es Salaam, baada ya kupata kidonda kwenye kidole chake cha mkono wa kushoto alipokuwa akibandua kucha za bandia alizobandikwa siku ya harusi yake na kusababisha apatwe na tetenasi.

Sophia hadi kifo kinamkuta alikuwa na umri wa miaka 28, Oktoba 15 alifunga ndoa na Richard Mmary katika harusi ya aina yake iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Wakisimulia namna walivyomuuguza Sophia kwa takriban wiki moja na nusu, mume wa marehemu anasema wiki moja baada ya sherehe ya harusi yao, Sophia aliamua kwenda tena salon kwa ajili ya kutengeneza nywele na kutoa kucha alizobandikwa siku ya harusi yao.

“Ilikuwa siku ya Jumamosi jioni, Sophia aliniaga anaenda saluni, alirudi baada ya saa mbili kupita lakini alikuwa akilalamika kuwa kidole kinamuuma sana, nikamuuliza amefanya nini akanijibu kuwa alikuwa anabandua kucha, lakini bahati mbaya kucha moja inaonekana ilibandikwa vibaya walipokuwa wanaibandua ilibanduka na ngoziya pembeni ya kidole na ikamuachia kidonda.

“Sikujali sana nikajua nikidonda cha kawaida tu,nikaenda kwenye duka la dawa nikamnunulia spiriti nikamsafisha lileeneo, lakini kilichonishangaza alikuwa akilalamikia maumivu makali,” anasema.

Mama yake Sophia, Victoria Haule anasema kuwa anaamini kuwa kifo cha mwanaye kimetokana na kucha bandia ambayo ilimsababishia apatwe na tetenasi.

“Tulipoona maumivu yanamzidia, tulimpeleka Hospitali ya Sinza, daktari alipomfanyia vipimo alitutaka tumpelekeHospitali ya Mwananyamala kwa matibabu zaidi, kwa kuwa alibaini kuwa Sophia ana tetenasiiliyosababishwa na kile kidonda.
Binafsi niliamini kucha ile ndiyo tatizo, kwa kuwa ilifikia hatua mkono mzima ukawa umevimba na kubadirika rangi na kuwa mweusi sana kama damu imevilia,” anasimulia mama yake Sophia.

Kwa maelezo ya nduguhao wa marehemu, Sophia alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu na kwa mujibu wa daktari kifo chake kilisababishwa na tetenasi.

Angalizo

Mabibi harusi wengi hivi sasa na hata wanawake kwa wasichana wanapendelea sana kubandika kucha bandia wakilenga kuboresha mwonekano wa vidole vyao.

Wengi hupenda kuwa na kucha ndefu ambazo huzipaka rangi na hivyo kuvutia pindi mtu azionapo.

Licha ya wao kuona kuwa kwa kufanya hivyo hupendeza, daktari mmoja wa magonjwa ya ngozi, anasema urembo wa kubandika kucha una athari zake kutokana na kutumika kwa gundi ambayo hunatahata kwenye ngozi.

Dk. Patrick Kashaija, wa Hospitali ya St. Benedict ya jijini Dar es Salaam, anasema amewahi kukutana nakesi za aina kama ya marehemu Sophia nyingi ambazo husababishwa na kubandikwa kucha za bandia.