Sekeseke la Okwi;TFF yaivimbia Yanga
Dar es Salaam. Siku moja baada
ya Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji kulipa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) siku saba kumaliza suala la mshambuliaji wao Emmanuel Okwi
aliyejiunga Simba, Shirikisho hilo limesema Yanga wasiwaamrishe kwani
wanafanya kazi kwa mujibu wa katiba na kanuni zao.
Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa aliliambia
gazeti hili jana kuwa kauli ya Yanga ni kichekesho kwa vile hawafanyi
kazi kwa kuamrishwa na Yanga na kuwataka watulie hadi hapo Kamati ya
Sheria na Haki za Wachezaji itakapokaa kujadili suala hilo.
“Tunafanya kazi kwa mujibu wa kanuni na taratibu,
hatufanyi kazi kwa kuamrishwa na mtu mmoja na isitoshe siyo suala lao tu
ambalo linatakiwa litolewe ufumbuzi, yapo mengi,” alisema Mwesigwa.
Juzi Manji alitoa siku saba kwa TFF kushughulikia
haraka suala lao na Okwi na kwamba zikimalizika siku saba bila ya
kupatiwa ufumbuzi atalifikisha suala hilo Fifa na ikibidi CAS.
Hata hivyo nakala ambayo gazeti hili linayo ambayo
imesainiwa na Katibu Mkuu wa TFF kwenda Yanga ya Agosti 26 ikiijulisha
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya mwanasheria Richard
Sinamtwa kukutana na uongozi wa Yanga kati ya Septemba 6 au 8 ili
kutatua suala la Yanga na mshambuliaji wao Emmanuel Okwi ambaye
amejiunga na Simba.
Katika madai ya Yanga ambayo wamewasilisha TFF ni
pamoja na Okwi kuisababishia klabu hiyo hasara ya dola 200,000 (zaidi ya
Sh300 milioni), klabu hiyo kupoteza ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara
baada ya Okwi kukacha kucheza mechi sita za ligi na mbili zikiwa za
kimataifa msimu uliopita. Pia, Yanga wanataka Okwi arudishe fedha zote
za mshahara ambazo walikuwa wakimlipa. Yanga ilikuwa ikimlipa
mshambuliaji huyo dola 4,000 kwa mwezi sawa na Sh 6.5 milioni.
Tayari Yanga imeshapeleka mashtaka yao TFF ikitaka
Okwi afungiwe kujihusisha na masuala ya soka nchini pamoja na kuishtaki
klabu ya Simba kwa kutangaza kumsajili Okwi na kumvalisha jezi ya Simba
wakati wakijua ana mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo ya Jangwani.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili ya Simba, Zakaria Hans Pope alisema, “Manji aache kuweweseka,
akumbuke Yanga walimsajili Okwi akiwa na mkataba na Etoile du Sahel na
unaisha mwaka 2015 hilo wanalijua wazi, lakini wakamsajili.”
“Sisi tulichofanya ni kumsaidia Okwi asipoteze
kipaji chake kama sheria za FIFA zinavyosema mchezaji hawezi kukaa nje
ya uwanja kwa miezi sita, tumemstiri hadi hapo matatizo yake na Yanga
yatakapomalizika.
“Kwanza nashangaa sana, Yanga wamemuacha huku roho
inawauma, kama una matatizo na mkeo unatakiwa umwambie aende kwa mama
yake akapumzike kisha wewe unajipima je, unaweza kuishi bila mke. Kama
unaweza unatoa talaka, sasa wao wametoa talaka huku mke wanamtaka si
kichekesho hicho roho zinauma. Okwi sasa hivi ni mali ya mwingine siyo
mali yao tena,” alisema Hans Pope.
Sekeseke la Okwi;TFF yaivimbia Yanga
Reviewed by CapchaMuzic
on
01:13:00
Rating: