Mganga amuua mwanaye kisa kazaliwa katanguliza makalio
MTOTO Regina Geofrey (miezi 14), ameuawa
kwa kunyongwa na baba yake mzazi Geofrey Kilingwa ‘Simbaiwe’ (27), kwa
madai alizaliwa akiwa ametanguliza makalio yake.
Baba wa binti huyo ambaye pia ni mganga
wa kienyeji anayeishi kitongoji cha Mwikang’ombe, Kijiji cha Katuma,
Mpanda, alitenda unyama huo kwa madai mtoto aliyezaliwa kwa kutanguliza
makalio ni mkosi na nuksi kubwa katika shughuli zake hizo za uganga wa
kienyeji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi,
Dhahiri Kidavashari, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, mzazi
huyo aliyetenda uhalifu huo Julai 20 mwaka huu ambako alikamatwa na
Jeshi la Polisi Agosti 26 mwaka huu.
Inadaiwa kuwa, siku hiyo ya tukio,
mtuhumiwa baada ya kumnyonga hadi kufa binti yake huyo, alimzika kwa
siri katika kibanda chake anachofanyia shughuli zake za uganga wa
kienyeji.
Akisimulia mkasa huo, Kamanda
Kidavashari alidai kuwa, mtoto Regina alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa
ambao haukufahamika kwa zaidi ya mwezi mmoja, ndipo Simbaiwe
alipolazimika kuanza kumuuguza kwa siri pasipo mkewe kufahamu, kwani
alimdanganya amepelekwa kutibiwa na babu yake huko Mwanza.
Inaelezwa kuwa, kibanda anachofanyia
kazi zake za uganga kiko mbali na makazi yake, hivyo ilikuwa rahisi
kumficha mtoto wake huyo kwa zaidi ya mwezi mzima akimtibu bila mkewe
kufahamu.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari,
wakazi wa kitongoji cha Mwikan’gombe wakiongozwa na Mwenyekiti wao,
walimtilia shaka mtuhumiwa kutokana na tetesi zilizozagaa eneo hilo
kuwa mtoto Regina alikuwa ameuawa na baba yake mzazi na kuzikwa kwa
siri.
Inadaiwa wakazi hao na Mwenyekiti wao,
walifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kuhoji alipo binti yake ambako
alipinga vikali, lakini alipopekuliwa kibandani kwake, walibaini kuweko
kwa tuta dogo lililokuwa limechimbwa siku za karibuni.
Kidavashari, aliongeza kuwa wakazi hao waliamua kufukua tuta hilo na kukuta kichwa cha mtoto huyo ndipo wakaitaarifu polisi .
Mama ya marehemu, Maria Exavery (22), alidai kuwa hakuhusishwa wala kupewa taarifa kwamba binti yake huyo amekufa.
“Mie nilikuwa nafahamu kuwa, Regina yuko kwa babu yake Mwanza akitibiwa,” alisema Maria.
Naye Regina Kaboni (40), mkazi wa
Isamilo Mwanza, ambaye alikuwa akitibiwa na mtuhumiwa, anadai kuwa
alishirikishwa katika maziko ya binti huyo.
“Hata hivyo…nilistushwa sana kwa kitendo
cha mtuhumiwa kumzika mwanaye bila ya kumshirikisha mkewe,
nilipomuuliza alidai kuwa kwa mila ya kwao, mtoto aliyezaliwa kwa
kutanguliza makalio, mama mzazi wa mtoto ni mwiko kushirikishwa katika
maziko ya mtoto huyo,” alidai.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, watu
wanne wakiwemo wazazi wa marehemu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi
kwa mahojiano zaidi na watafikishwa mahakamani mara tu baada ya
upelelezi wa awali kukamilika.
Wengine wanaoshikiliwa na Polisi ni Regina Kaboni ni Msolwa Jacob (29), mkazi wa kitongoji cha Mwikang’ombe.
Mganga amuua mwanaye kisa kazaliwa katanguliza makalio
Reviewed by CapchaMuzic
on
11:42:00
Rating: